Waters of Life

Biblical Studies in Multiple Languages

Search in "Kiswahili":
Home -- Kiswahili -- John - 028 (Jesus leads the adulteress to repentance)
This page in: -- Albanian -- Arabic -- Armenian -- Bengali -- Burmese -- Cebuano -- Chinese -- Dioula -- English -- Farsi? -- French -- Georgian -- Greek -- Hausa -- Hindi -- Igbo -- Indonesian -- Javanese -- KISWAHILI -- Kyrgyz -- Malayalam -- Peul -- Portuguese -- Russian -- Serbian -- Somali -- Spanish -- Tamil -- Telugu -- Thai -- Turkish -- Twi -- Urdu -- Uyghur? -- Uzbek -- Vietnamese -- Yiddish -- Yoruba

Previous Lesson -- Next Lesson

YOHANA - Nuru inaangaza gizani
Somo la Injili ya Kristo kufuatana na Mtume Yohana
SEHEMU YA 1 - Kuangaza kwa nuru tukufu ya Mungu (Yohana 1:1 - 4:54)
C - Kristo kutembelea mara ya kwanza mji wa Yerusalemu (Yohana 2:13 - 4:54) -- Neno Kuu: Kuabudu kwa kweli ni nini?
4. Yesu atembelea Samaria (Yohana 4:1–42)

a) Yesu anamwongoza mwanamke mzinzi apate kutubu (Yohana 4:1-26)


YOHANA 4:1-6
1 “Kwa hiyo Bwana alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana 2 Mbatizaji na kuwabatiza (ila Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake) 3 aliacha Uyahudi, akaenda tena zake mpaka Galilaya. 4 Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria. 5 Basi akafika kunako mji wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. 6 Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu alichoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.”

Mwinjilisti anamwita Yesu “Bwana”, yeye atawalaye kama Mfalme wa milele juu ya historia ya ulimwengu. Yeye awezaye kuhukumu na kutoa neema. Ni yeye awaongozaye, pia na kuamua yote. Yohana aliona utukufu wake na kumheshimu na cheo hiki cha kutawala, “Bwana”.

Mafarisayo walikuwa wameanza kuchochea, tayari kuanza vita naye. Mahubiri ya Yesu hapo Uyahudi ulikuwa mafanikio ya kuleta nuru. Aliwaita watu watubu, wakikiri dhambi zao, jinsi alivyofanya Mbatizaji. Ilikuwa kana kwamba amepokea zamu kutoka kwake Mbatizaji (ingawa mwenyewe hakubatiza, ila aliwaachia wanafunzi wake, maana walikuwa wametokana na kundi la Yohana Mbatizaji). Yesu alifundisha kwamba, ubatizo wa maji peke yake si kitu, ila ni alama kwa ubatizo wa kiroho. Hata hivyo, saa yake ilikuwa bado, wala mwenyewe hakubatiza.

Wakati ushindani wa Mafarisayo ulipoendelea kuzidi, Yesu akaondoka kwenda kaskazini. Aliishi kufuatana na mipango ya Babaye. Wakati wa kukabiliana na hao wanasheria waziwazi ilikuwa bado. Yesu akapendelea kusafiri kupitia nchi za milima na kuingia Samaria, ndiyo njia fupi kufika Galilaya.

Hao Wasamaria hawakuwa watu wa kutambulikana ndani ya Agano la Kale, kwa sababu walikuwa kundi walio changamana na wananchi wa Kanaani. Wakati Waashuru walipopiga vita na kushinda Samaria mwaka 722 BC (kabla ya Kristo), wakiwapeleka wengi wa uzao wa Ibrahimu hadi Babeli, katika nchi ya Mesopotamia, wakaleta watu wengine waishi Samaria. Hivyo kuchanganyikana kulitokea, kulicholeta na kuchanganya imani.

Yesu alifikia Sikari, karibu na Shekemu, palipokuwa ni pa kufikia kwa Babu wa zamani, Ibrahimu na ukoo wake. Pia ilikuwa mahali Yoshua alipofanya mapatano ya Waisraeli na Mungu wao baada ya kuingia Kanaani. (Mwanzo 12:6 na Yoshua 8: 30-35). Kulikuwa na kisima cha zamani karibu, kilichoaminiwa ni cha Yakobo (Mwanzo 33:19) Mifupa ya Yusufu iliyoletwa nao toka Misri ilikuwa ilizikwa mahali hapo karibu (Yoshua 24:32). Sehemu hii ya nchi ilipata kuwa na historia katika Agano la Kale.

Yesu aliketi kando ya kisima, akiwa amechoka kutokana na safari ndefu na jasho la saa za mchana. Alikuwa ni mwanadamu kamili, mchovu na mwenye kiu, sio kama mtu aliyeonekana katika njozi tu au katika hali ya ki-mungu, hapana - mwanadamu mwenye alama zote za kibinadamu na za udhaifu wake.

YOHANA 4:7-15
7 „Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. 8 Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. 9 Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria) 10 Yesu akajibu akamwambia, Kama ungalijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. 11 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? 12 Je, wewe u mkubwa kuliko baba yetu Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia na wanyama wake? 13 Yesu akajibu akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena. 14 Walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele. 15 Yule manamke akamwambia, Bwana, nipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.“

Wakati Yesu aliposimama karibu na kisima, mwanamke Msamaria akaja kuteka maji. Hakuja asubuhi au jioni kama wanawake wengine, lakini mchana. Hakutaka kukutana na wengine; kwa ajili ya sifa yake mbaya alidharauliwa na wote kila mahali alikoenda. Yesu alitambua moyo wake wenye shida tokea mbali, akasikia kiu chake cha kusafishwa. Aliamua kumsaidia. Hakumtajia Amri Kumi, wala hakumkemea, bali kwa urahisi akamwomba maji anywe. Alimchukua kuwa mtu aliyehitaji kumtolea kinywaji. Lakini alipomtambua kwamba ni Myahudi, alisita. Maana kulikuwa na korongo ya chini kati ya watu wake na wao. Ilikuwa kiasi cha pande zote mbili wasithubutu kugusa vitu vyao kwa hofu ya kuwa najisi. Hata hivyo, Yesu akamwelekea kana kwamba hakuna kizuizi cha kawaida kati yao, akamheshimu kwa kuomba kitu kwake.

Kusudi la Kristo ilikuwa ni kuamcha njaa kwa Mungu ndani ya mtenda dhambi huyu. Kwa vili mazingira yalikuwa ya kisimani, ilifaa aongee naye habari ya maji. Hii iliamsha ndani yake hamu ya kipawa cha Mungu. Aliweka mbele zake upendo wa Mungu kama shabaha. Siyo hukumu iliyomngojea ya kupotea, bali ilikuwa ni zawadi ya Mungu iliyoandaliwa kwake katika neema. Je, si mwujiza wa ajabu jambo hilo?

Neema haiji hivihivi toka peponi, bali inakuja kipepee katika nafsi ya Yesu. Yeye ndiye mtoaji wa vipawa na neema tukufu. Bado mwanamke huyu alimwangalia kama mtu wa kawaida. Utukufu wake Kristo bado ulifichwa machoni pake, lakini upendo wake safi uling’aa wazi mbele zake. Akamwambia kwamba anao uwezo wa kugawa maji ya uzima. Hiki kinywaji cha mbinguni alichokitoa, kilikuwa na uwezo wa kuzimisha kiu cha moyo. Watu wote hutamani upendo na ukweli, wakiwa na shauku ya kurudi kwa Mungu. Yeyote ajaye kwake Yesu, atapata kutuliza kiu chake.

Yesu huwa anatoa zawadi ya Mungu kwao wanaoiomba. Tunatakiwa kukiri haja zetu, jinsi Yesu alivyotamka hamu yake ya maji ya kunywa. Bali asiyekubali kuinamisha kichwa chake na kuomba, hatapokea maji ya mbinguni yanayoweza kutolewa bure.

Yule mwanamke alikosa kumwelewa Yesu. Akaitika kwa maneno ya wazi: „Huna chombo cha kutekea, na kisima ni kirefu, basi utawezaje kunipatia maji?“ Wakati uo huo alishangazwa alipoona wema na upendo wake Yesu. Kinyume cha majirani yake hakumdharau kabisa. Alimtambua yu mbali naye kwa enzi yake, lakini akampenda katika utakatifu wake. Wakati wowote hajakutana na mtu safi kama yeye. Basi akamwuliza: “Wewe ni mkubwa kuliko baba yetu Yakobo? Unakusudia kufanya mwujiza wa kutupatia kisima kipya?”

Bwana Yesu akamjibu akimweleza kwamba hazungumzi maji ya kawaida, maana yeyote anayezimisha kiu chake kimwili kwa maji ya kawaida atapata kuona kiu tena. Mwili hupokea maji na kuyatoa tena. Bali Yesu hutupatia maji yaliyo hai na hivyo kuridhisha kila kiu cha kiroho. Wakristo humtafuta Mungu na kumpata. Hao sio wanafilosofia wa kutafakari habari za ukweli bila kuufikia. Mungu aliwaona; wao wanapata kumtambua kweli kweli. Upendo wake daima inawatosheleza. Mafunuo yake hayawachoshi wala hayawezi kupitwa na wakati, lakini yanabubujika daima, yakiwa mapya kila kukicha na kuburudisha ufahamu wetu juu ya Mungu. Hayo siyo ya kimawazo tu, bali ni nguvu, uhai, nuru na amani moyoni. Roho Mtakatifu ndiye kipawa cha Mungu cha maji ya mbinguni.

Mara tatu Yesu anarudia thibitisho kwamba, yeye pekee ndiye mtoaji wa maji ya uhai. Si dini yoyote au chama, wala si ukoo au urafiki unaoweza kuzimisha kiu cha roho yako, ni Yesu pekee aliye Mwokozi wako.

Yeyote atakayepokea zawadi hiyo ya Mungu atapata kubadilishwa. Mwenye kiu atakuwa chemchemi ya maji yanayofurika kwa ajili ya baraka kwa wengine, akiwapa neema, furaha na upendo pamoja na matunda mengine ya kiroho. Kwa kudumu ndani ya Kristo tunapokea neema juu ya neema, na hivyo kuwa zawadi ya Mungu kwa watu wengine wengi.

Mwanamke yule akasikia kwamba, Yesu alikuwa wa kweli katika maongezi yake naye wala sio mchawi. Basi akataka kwake maji yale ya uzima. Alikiri haja yake, lakini aliendelea kuwaza kwamba Yesu bado anasema habari ya maji ya kawaida. Alifikiri kwa kupokea maji hayo asingehitaji tena kubeba ndoo ya maji kichwani na kuhangaika na wale waliomdharau.

SALA: Bwana Yesu, mtoaji wa maji ya uzima, zimisha kiu chetu cha kukufahamu zaidi na kukupenda. Uwe radhi na kuchafua kwetu; tusafishe na aina zote za uchafu, ili Roho Mtakatifu aweze kutujia na kutulia ndani yetu daima. Tupate kuwa chemchemi za maji, ili wengi wapate kunywea yanayobubujikia Roho yako. Tufundishe unyenyekevu, maombi, upendo na imani. Amina.

SWALI:

  1. Jambo gani ni zawadi anayotupatia Yesu? Na ni namna gani tabia na sifa zake?

www.Waters-of-Life.net

Page last modified on July 24, 2013, at 07:56 AM | powered by PmWiki (pmwiki-2.3.3)